Timu zinazoshiriki katika Afcon 2019
Alhamisi, Juni 20, 2019
Timu zinazoshiriki katika Afcon 2019

Kwa mara ya kwanza, katika historia ya soka la bara hili, fainali za mwaka huu zitafanyika katikati ya mwaka, yaani kati ya mwezi Juni na Julai na si Januari - Februari kama ilivyozoeleka.

Egypt (The Pharaohs)

Wenyeji wa mashindano. Mabingwa wa kihistoria. Wajukuu wa Farao au ‘The Pharaohs’ kama wanavyofahamika bila shaka ndio wababe wa soka la Afrika.

Wenyeji wa mashindano. Mabingwa wa kihistoria. Wajukuu wa Farao au ‘The Pharaohs’ kama wanavyofahamika bila shaka ndio wababe wa soka la Afrika.

Safari hii wana matumaini makubwa ya kufanya vyema zaidi, macho na imani yao yakimwelekea Salah, ambaye amekuwa mkombozi wao katika siku za hivi karibuni.

 Senegal (The Lions of Teranga)

Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2018, Senegal ilikuwa timu bora Afrika, kwa mujibu wa viwango vya FIFA. Simba hawa wa Teranga, wana nafasi kubwa ya kutwaa taji hili, wakiongozwa na nahodha wao, Straika wa Liverpool, Sadio Mane.

Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2018, Senegal ilikuwa timu bora Afrika, kwa mujibu wa viwango vya FIFA. Simba hawa wa Teranga, wana nafasi kubwa ya kutwaa taji hili, wakiongozwa na nahodha wao, Straika wa Liverpool, Sadio Mane.

Tunisia (The Carthage Eagles)

Kwa sasa, Tunisia inaongoza kwa ubora Afrika. Kikosi cha The Carthage Eagles, hakina staa hata mmoja, wote ni wachezaji wa kawaida lakini wakali na wanaelewana.

Ukimtoa Naim Sliti, anayeichezea Dijon FC ya Ufaransa, wengine wote wanacheza kwenye ligi ya ndani. Kila mtu katika kikosi hicho ana ndoto ya kupata mafanikio. Hii ndio silaha yao kubwa. Wanajuana.

Nigeria (The Super Eagles)

Huko nyuma walikuwa wababe wa soka la Afrika. Walitawala kila idara, hakuna aliyetamani kukutana nao. Baadaye wakawa laini, hadi Kenya ilikuwa inawatambia.

Kwa kifupi Super Eagles ilipoteza nguvu za kupaa angani. Mwaka jana ilikuwa gumzo kwenye fainali za Kombe la Dunia, zilizofanyika Ufaransa. Sio kutokana ukali wa kikosi, bali uzuri wa jezi yao.

Kila mtu alikuwa anaitaja Nigeria, hatimaye ikaishia kuuza jezi. Ikiwa na mastaa kama Ahmed Mussa, nahodha John Obi Mikel, Alex Iwobi na Wilfred Ndindi, inaenda Misri, ikiwa na lengo moja tu, sio kuuza jezi bali kutwaa taji, itaweza? Sijui

Algeria (The Desert Warriors)

Maarufu kama wababe wa Jangwani, kila mtu anaiogopa Algeria. Ipo Kundi C pamoja na Senegal, Kenya na Tanzania. Mechi yake ya kwanza, itakuwa Juni 23, dhidi ya Kenya. Baada ya hapo itakutana na Senegal.

Maarufu kama wababe wa Jangwani, kila mtu anaiogopa Algeria. Ipo Kundi C pamoja na Senegal, Kenya na Tanzania. Mechi yake ya kwanza, itakuwa Juni 23, dhidi ya Kenya. Baada ya hapo itakutana na Senegal.

Kama ilivyo kwa Tunisia, sehemu kubwa ya wachezaji wa Algeria wanajuana na kuelewana kiuchezaji. Wameshiriki fainali mara 18 na kushinda mara moja tu. Huu utakuwa mwaka wao?

Ghana (The Black Stars)

Mbali na Senegal, The Black Stars ni timu nyingine iliyotinga robo fainali ya Kombe la Dunia, katika historia ya soka katika bara hili.

Hii inaifanya Ghana kuhofiwa Sana licha ya kutwangwa 1-0 na Kenya kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya kufuzu AFCON, iliyopigwa jijini Nairobi.

Kikosi cha Black Stars, kinachonolewa na Kocha Kwasi Appiah, kinajivunia uwepo wa ndugu wawili, Jordan na Andre Ayew ambaye amepewa unahodha wa kikosi. Kwa jumla imeshiriki fainali hizi mara 22, ikishinda mara nne. Jahazi lake litaongozwa vyema na nahodha wa wa jumla, Asamoah Gyan? Muda utasema.

Ivory Coast (The Elephants)

Inapotajwa Ivory Coast, jina linalokuja akilini ni jina la nyota wa zamani wa Chelsea, Didier Drogba. Huyu alikuwa zaidi ya straika na nahodha ndani ya kikosi cha The Elephants, alikuwa kiongozi. Bado ina wachezaj wazuri tu.

Katika kikosi chake, inaenda Misri ikiwa na uhakika wa kutwaa taji hili kutokana na uwepo wa miguu ya straika wa Crystal Palace, Wilfred Zaha na nyota wa Fulham, Jean Michael Seri. Tembo hawa wamebeba kombe hili mara mbili, katika mara 22, walizoshiriki.

Cameroon (The Indomitable Lions )

Mabingwa watetezi, Cameroon, wanaelekea Misri wakiwa na morali na hamu ya kula nyama. Simba wasioshindika, wanaenda Cairo chini ya uongozi wa Waholanzi Clarence Seedoff na Patrick Kluivert, wakiwa na lengo la kutetea taji lao.

Kikosini kina makipa watatu wazoefu. Yupo mkongwe, Carlos Idriss Kameni, kinda Andre Onana (Ajax) na Fabrice Ondoa (Oostende), aliyesimama langoni dhidi ya Gabon, ilipotwaa taji hili miaka miwili iliyopita.

Morocco (The Atlas Lions)

Kama ilivyo kwa timu nyingi za mataifa ya Kiarabu, Morocco ni maarufu kwa kutandaza soka safi. Mwaka jana ilikuwa miongoni mwa mataifa matano yaliyowakilisha Afrika, kwenye Kombe la Dunia.

The Atlas Lions, wanaenda Misri wakijivunia uwepo wa winga teleza wa Ajax, Hakim Ziyech na nahodha Medhi Benatia, anayeichezea Al - Duhail, katika kikosi hicho. Imeshiriki mara 16 na kulitwaa mara moja tu. Itafanya nini? Tusubiri pia.

DR Congo (The Leopards )

Wanaenda Misri, wakiwa na matumaini vyema zaidi ya miaka miwili iliyopita, wakiwategemea nyota wa Anderlecht Yannick Bolasie, na Arthur Masuaku wa West Ham, kuwabeba. Watawalazimisha wapinzani wao, kucheza Ndo

Mali (The Eagles)

The Eagles imeshiriki fainali za AFCON mara 10, katika historia ya soka lake, lakini haijawahi kuonja ladhaa ya ubingwa. Huko Misri itawategemea nyota wake, Adama Traore (Cercle Brugge) na Moussa Marega (FC Porto.

Africa Kusini (Bafana Bafana)

Kuanzia mwaka 2010, ilipoandaa fainali za Kombe la Dunia, soka la Afrika Kusini limeimarika sana na itakuwa dhambi kuidharau. Bafana Bafana inaenda Misri kufanya kweli.

Itatua Cairo, na lengo la kuishangaza Afrika, kwa kubeba kombe hili kwa mara ya pili, huku ikijivunia uwepo wa Piercy Tau wa Saint - Gilloise ya Belgium na Hlompho Kekana (Mamelodi Sundown). Mara ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa ni 1996.

Guinea (National Elephants)

Hii ni mara yake ya 12. Katika mara zote 11, ubingwa umekuwa mfupa mgumu kuutafuna. Tembo hawa wa Taifa la Guinea, walimaliza wa pili, nyuma ya vinara Ivory Coast, kwenye Kundi H. Watawategemea Naby Keita (Liverpool) na Ibrahima Cisse (Fulham), kuwabeba

Kenya (Harambee Stars)

Mara ya mwisho Kenya ilishiriki fainali mwaka 2004. Miaka 15 baadaye imerudi tena, safari hii chini ya Mfaransa, Sebastien Migne, ambaye ameonyesha uwezo mkubwa. Hivi sasa iko kambini jijini Paris, Ufaransa.

Pamoja na ukweli ilifuzu baada ya Sierra Leone kuondolewa mashindanoni, Harambee Stars imedhamiria kufanya vizuri katika Kundi C, ambako wamepangwa pamoja na Algeria, Senegal na majirani zao Tanzania. Itaweza? Muda utasema.

Uganda (The Cranes)

Inaongoza kwa ubora katika Ukanda wa Afrika Mashariki. Ilishiriki fainali za mwaka juzi. Ilikuwa vinara wa kundi lake, juu ya Tanzania. Katika kikosi cha The Cranes, yupo kipa wa Mamelodi Sundowns, Dennis Onyango, Khalid Aucho (Churchill Brothers) na Emmanuel Okwi wa Simba.

Benin (The squirrels)

The Squirrels, imeshiriki fainali hizi mara tatu, lakini mara zote imeishia kwenye makundi.

Hii ikiwa ni mara yake ya nne, huenda ikaja kivingine hasa ikizingatiwa kuwa kikosi chake kinaundwa na mastaa kibao, wakiwemo nyota wa Huddersfield United, Steve Mounie na beki wa Lens, Djiman Koukou.

Mauritania (The Lions of Chinguetti)

Mauritania imefuzu AFCON kwa mara ya kwanza. Simba wa Chinguetti, wapo kwenye nafasi ya 101, kwenye viwango vya FIFA, huenda wakajaribu kupambana na kuonesha dunia uwezo wao wa kisoka. Mastaa wao ni Moulaye Besam (AS Gabes) na Hassan El Ide (Real Valladolid.

Namibia (The Brave Warriors)

Hii ni fainali yake ya tatu. Wapambanaji wasiogopa, hawajawahi vuka hatua ya makundi. Wakiwa na wachezaji wazuri wanaokipiga kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini na Ligi ya Serbia, akiwemo Henrik Somaeb (Zemun) na Deon Hotto (Golden State Arrows), huenda wakafanya maajabu.

Madagascar (Barea)

Madagascar pia watakuwa wanashiriki AFCON kwa mara ya kwanza. Taifa hilo lililopo kwenye kisiwa, linajivunia kuwa na mastaa kadhaa kama Faneva Ima Andriatsima (Clermont Foot, Ufaransa) na Arohasina Andrianarimanana (Kaizer Chiefs, Afrika Kusini). Barea wamekuja na jipya gani?

Tanzania (Taifa Stars)

Baada ya kukaa nje kwa kipindi cha miaka 39, hatimaye Tanzania imerejea kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika. Taifa Stars inayonolewa na nyota wa zamani wa Nigeria, Emmanuel Amunike imerudi na kiburi, inajiamini pia.

Ikiwa katika Kundi C, pamoja na Algeria, Senegal na majirani zao Kenya, inajivunia uwepo wa nahodha wake na straika wa KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta, ambaye msimu huu ameiongoza Genk kutwaa taji la Ligi Kuu ya Ubelgiji, akitupia kambani mabao 23.

Zimbabwe (The Warriors)

Zimbabwe itakuwa inashiriki fainali hizi kwa mara ya pili mtawalia na ya tatu katika historia ya soka lake. Ilikuwepo kwenye fainali za 2017, zilizofanyika Gabon. Huenda itakuwa imejifunza kutokana na makosa ya mwaka juzi.

Labda Safari hii, itapiga hatua zaidi. Wachezaji inaowategemea ni Marvelous Nakamba (Club Brugge) na Knowledge Musona (Anderlecht.

Guinea-Bissau (Djurtus)

Kama ilivyo kwa Zimbabwe, Guinea Bissau pia itakuwa inashiriki kwa mara ya pili mfululizo. Mwaka 2017 iliishia kwenye hatua ya makundi. Mwaka huu, ina imani kwa nyota wake, Frederick Mendy (Vitoria de Setubal, Ureno) na Zezinho Djafal (FK Senica, Slovakia), watawavusha.

Angola (Giant Sable Antelopes)

Angola, imeshiriki fainali hizi mara saba. Hata hivyo, bado inahaha kutwaa taji lake la kwanza.

Mastaa wake ni Djalma Campo (Alanyaspor, Turkey) na Herenilson (Petro de Luanda, Angola). Vipi nafasi yake?  Muda ni msema kweli.

Burundi (The Swallows)

Hii ni fainali yake ya kwanza. Kila mtu anawachukulia poa, jambo ambalo, Saido Berahino (Stoke City), na Fiston Abdul Razawa (JS Kabylie), sidhani kama wanalifurahia.