Kilichoibeba Algeria Afcon
Jumapili, Julai 21, 2019
Kilichoibeba Algeria Afcon

Uimara na ubora wa Algeria kuanzia safu ya ulinzi hadi ushambuliaji, nidhamu ya kimbinu, kujitolea kwa wachezaji na uhodari wa kocha Djamel Belmadi vimechangia kwa kiasi kikubwa kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) nchini Misri.

Bao la mapema katika dakika ya pili la mshambuliaji Baghdad Bounedjah, lilitosha kuwazamisha Senegal na kuipatia Algeria taji hilo kwa mara ya pili baada ya kufanya hivyo 1990.

Dalili za ubingwa kwa Algeria zilianza kuonekana mapema kutokana na kiwango bora ambacho timu hiyo ilianza kuonyesha katika mechi ya kwanza ya hatua ya makundi dhidi ya Kenya walipoibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Algeria ilikuwa na muunganiko bora wa kitimu kuanzia kwenye safu ya ulinzi hadi ushambuliaji ambao ulikuwa chachu kwao kutamba kwenye fainali hizo.

Ilikuwa na safu imara ya ulinzi ambayo haikuwa inafanya makosa ya mara kwa mara na kuwaruhusu wapinzani wao kulifikia lango lao kirahisi na kwa kulidhihirisha hilo hadi inafika fainali ilikuwa imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili.

Vilevile, washambuliaji wake walikuwa tishio katika kuzifumania nyavu na kulazimisha mabeki wa timu pinzani kufanya makosa, wakipachika jumla ya mabao 13 ambayo ni idadi kubwa zaidi ya magoli kufungwa na timu moja kwenye mashindano hayo.

Mbali na hilo, safu yake ya kiungo ilifanya kazi kubwa kusaidia ulinzi kwa kuvunja mipango na mashambulizi ya timu pinzani, lakini pia kutoa sapoti kwa washambuliaji na kuwachezesha wenzao, jambo lililotengeneza ‘balansi’ ya kitimu na ushahidi wa hilo viungo Adlene Guediola, Soufiane Feghouli na Ismaer Bennacer walipiga pasi 674, walitengeneza nafasi 14 na kupora mipira kwa wapinzani mara 16.

Takwimu zinaonyesha kuwa Algeria ndio timu iliyokuwa kinara wa kutumia nafasi ilizotengeneza, kufunga mabao ikiwa na asilimia 20, imekuwa kinara wa kupachika idadi ya mabao (13) na pia ndio timu iliyoruhusu nyavu zake zitikiswe mara chache zaidi ambapo imefungwa mabao mawili.

Lakini hilo lilichangiwa na namna wachezaji wake walivyofanyia kazi mbinu za kocha Belmadi hasa ile ya soka la kasi na kuwabana wapinzani kuanzia eneo lao na kuwalazimisha wafanye makosa ili wasipate nafasi ya kutengeneza mashambulizi.

Belmadi mbali na kupendelea kutumia mbinu hiyo, ni kocha ambaye hubadilika haraka kimbinu anapogundua mpinzani ameng’amua mbinu zake, jambo ambalo lilikuwa likiwaweka kwenye wakati mgumu makocha wa timu pinzani.

Mbali na hayo, Algeria walikuwa na kikosi kinachocheza kitimu na kwa kudhihirisha hilo, wachezaji wawili wa kikosi chake wamepata tuzo kwenye fainali hizo ambao ni Ismaer Bennacer - aliyechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mashindano pamoja Rais M’bolhi ambaye ni kipa bora wa Afcon 2019.

“Ubingwa huu una ladha ya kipekee kwa sababu tumetwaa huku tukiwa hatujachezea nyumbani,” alisema kocha Belmadi, baada ya kipenga cha mwisho.

Mwananchi